Unaupataje muda wa kuandika kitabu?
Swali gumu ambalo kila mtu anayetaka kuandika kutabu hujiuliza ni, “napataje muda wa kuandika kitabu? Majibu ya swali hili si magumu wala si mepesi kwa sababu kila mtu ana masaa yale yale 24 lakini kuna mwingine ataweza kuandika kitabu na mwingine atashindwa kuandika kitabu.
Tuna mambo mengi tunayofanya na yote yanataka nafasi ya kufanyika ndani ya haya masaa 24 tuliyonayo. Pengine nukuu ya Toni Morrison inayosema “Write at the edges of the day.” Inaweza kutupa mwanga wa kuanzia kujibu swali hili la kuupata muda wa kuandika kitabu. Ki msingi anachosema Toni ni kuwa, unaweza pata muda wa kuandika kitabu chako mwanzoni mwa siku au mwishoni kwa siku.
Mwanzoni au mwishoni kwa siku.
Kama wewe ni mtu wa kuamka mapema sana kujiandaa kwenda kwenye majukumu yako ya siku, basi muda wa asubuhi sana ndiyo unaweza kuutumia kuandika kitabu. Hii inawafaa sana watu walioajiriwa wanaotaka kuandika kitabu. Mwandishi wa Vitabu Joanna Penn amewahi kutumia mbinu hii, anasema kuwa “Niliandika kitabu changu cha kwanza nilipokuwa mwajiriwa. Nilikuwa naamka saa kumi na moja alfajiri, na baada ya kujiandaa kwenda kazini, nilikaa kuandika kitabu kwanza kwa sababu kazini nilikosa muda na baada ya kutoka kazini nisingeweza kuandika kwa sababu ya uchovu.
Si kila mtu ataweza kuandika asubuhi sana anapoamka, kuna wengine wataweza kuandika muda wa usiku baada ya kutoka kazini. Binafsi, nimeandika baadhi ya vitabu vyangu wakati wa usiku nikiwa nimetulia.
Kwa hiyo, siku inapoanza unaweza kuandika kitabu au siku yako inapoisha unaweza kuandika kitabu pia.
Kitu gani unaweza kukiachilia au kukiacha ili upate muda wa kuandika?
Umeshindwa kupata muda asubuhi au usiku, nini ufanye sasa? Angalia katika vitu unavyofanya mchana, kipi ukiache ili utengeneze muda hapo wa kuandika kitabu. Mfano, kama unaangalia TV kwa masaa matatu, punguza muda hapa, angalia TV kwa lisaa limoja tu na masaa mawili yanayobakia yatoe kuandika kitabu.
Kama upo kazini, ule muda wa kupiga soga na wenzio wakati mmejipumzisha, wewe utumie kuandika kitabu.
Vipi ule muda upo kwenye gari au daladala?
Muda mwingi unapotea tunapokuwa kwenye gari au daladala kwa sababu ya, mfano, foleni. Muda huu unaweza kuutumia kuandika kitabu pia. Kama upo kwenye foleni masaa mawili, fikiria ni kurasa ngapi utakuwa umeweza kuandika? Bila shaka nyingi sana.
Jambo la muhimu ni nini?
Muda unatengenezwa! Jambo lolote ukitaka kulifanya lazima utalitengenezea muda wa kulifanya. Joann Penn anasema “it’s all about scheduling”. Ni wewe tu kuweka ratiba na kuamua kuifuata. Pangilia muda wa kuandika kitabu na hakikisha unautumia kuandika.