#Kitabukipya: Mtitu aachia kitabu kipya tena.
Mwandishi wa vitabu, Meinrad Mtitu ameachia kitabu kipya tena kinachokwenda kwa jina la Kiongozi Aliyechoka. Pata kionjo cha kitabu hiki katika muhtasari ufuatao;
Pengine moja ya eneo ambalo halizungumzwi sana ni kuhusu uchovu wa viongozi. Hii inachangiwa na dhana potofu ya kuwaona viongozi kama “wanadamu wasio wa kawaida” ambao kuchoka hakuwahusu. Lakini ukweli ni kwamba viongozi ni wanadamu wa kawaida ambao wanachoka, na pengine ndio wanaochoka kuliko wale wanaowaongoza. Uchovu ni kuchakaa kwa nguvu za kimwili, Kihisia, Kiakili na Kiroho kunakosababishwa na jitihada za muda mrefu. Ufahamu wa watu wengi juu ya uchovu upo zaidi katika eneo moja tu, la kuchoka kimwili. Kuna maeneo makuu manne ambayo uchovu huweza kumuathiri kiongozi katika maisha yake ya kila siku ya kumtumikia Mungu, kwa kupitia huduma mbalimbali anazofanya. Maeneo haya ni kimwili, kiakili, kihisia, na kiroho.
Tunaishi katika ulimwengu uliojaa viongozi waliochoka, mfumo wa maisha umepelekea kuwa na viongozi wa namna hii, na wengi hufa mapema kwa sababu ya kuchoka. Kutokana na shinikizo la maisha na kutaka kufanikiwa wengi huteketeza na kupoteza nguvu zao kwa kasi. Majukumu ya kihuduma tunayofanya kila siku yananyonya na kuteketeza nguvu zetu (kimwili, kihisia, kiakili na kiroho) na kama hatuna maarifa ya kuzirejeza tutajikuta kwenye hali ya uchovu kisha kuteketea kabisa kwa nguvu. Hali hii itaathiri afya zetu, akili zetu, hisia na roho zetu pia.
Kiongozi anayesumbuka na kuteseka na uchovu sugu atahisi kupungukiwa kwa nguvu za kimwili na kiakili, kuwa na maumivu na kuumwa, kuwa na hali ya kuchukia huduma au utumishi anaoufanya, atakuwa kuwa mbali kiakili katika huduma, akili yake haipo katika huduma na ataonekana kutojali. Na kama hiyo haitoshi, atakuwa na hisia za kupita kiasi za kujioana hana matumaini, amepoteza na ameshindwa. Kiongozi anayeteseka na hali ya uchovu au anayehisi kuwa mchovu kihisia au kiakili hali hii inaweza kumpelekea katika tabia zisizofaa, hata kuchanganyikiwa kiakili na kuwa dhaifu kimwili , kuharibikiwa na hata kupelekea kifo cha mapema.
Kila kiongozi anapaswa kujilinda na hali hii kwa kujua dalili za uchovu na tiba yake, na nini afanye kuzijereza nguvu zake pale zinapoteketea.