Jinsi ya kujenga jukwaa lako kama mwandishi - 1
Kati ya mambo mengi yanayowatatiza waandishi wengi wa vitabu ni kujua maana ya jukwaa la mwandishi ni nini? na jinsi ya kulijenga jukwaa lako kama mwandishi ili kuuza vitabu vyako. Kwa sababu hili ni jambo muhimu kujua, chapisho la leo litajikita kueleza hili kwa kina;
Jukwaa la mwandishi ni nini?
Vile wasomaji wanavyokufikia wewe kupata kazi zako au vile wewe unavyopatikana kwa wasomaji humaanika kama jukwaa la mwandishi. Jukwaa la mwandishi ni namna zote na njia zote utauza vitabu vyako kwa wasomaji. Kila mwandishi ana jukwaa lake tofauti na mwandishi mwingine hivyo majukwaa mawili hayawezi kufanana kwa waandishi wawili. Kwa kifupi ni kuwa, vile mimi nitauza vitabu vyangu inaweza kuwa tofauti na vile wewe utauza vitabu vyako.
Jukwaa la mwandishi linaweza kuwa ni watu wanaokufatilia wewe (mashabiki) katika mtandao wa kijamii unaotumia, mfano Facebook au Instagram. Jukwaa la mwandishi linaweza kuwa orodha ya watu ulionao katika mtandao wa WhatsApp au orodha ya baruapepe za watu wako ulionao.
Mifano ya jukwaa la mwandishi
Kama nilivyosema kuwa, jukwaa la mwandishi halifanani kati ya mwandishi mmoja na mwingine. Kwa mfano, msanii anayetoa kitabu anaweza asiwe na orodha ndefu ya baruapepe za watu wanaomfatilia lakini akawa na mashabiki wengi katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, kwa hiyo huyu msanii jukwaa lake kama mwandishi litakuwa mtandao wa kijamii na wasomaji watapata kitabu chake hapo.
Au, mhadhiri wa chuo fulani anaweza asiwe na mashabiki wengi katika mtandao wa kijamii lakini akawa anajulikana zaidi katika fani yake anayofundisha (mtalaamu), hivyo katika mtandao wake wa kujulikana (watu wengi wanaomjua) ndiyo itakuwa jukwaa lake kama mwandishi na ataweza kuuza nakala nyingi zaidi kuliko kutumia mtandao wa kijamii.
Au, kuna mwandishi ambaye hajulikani sana na watu lakini ana amefanikiwa kupata orodha kubwa ya baruapepe za watu wanaomfatilia. Mwandishi kama huyu, jukwaa lake litakuwa ni hiyo orodha ya baruapepe alizonazo na ataweza kuuza huko zaidi kuliko kutumia mtandao wa kijamii.
Unajengaje jukwaa lako kama mwandishi?
Katika mifano ya hapo juu, nimegusa mambo matatu, mashabiki wengi ulionao katika mtandao wa kijamii, kujulikana zaidi katika eneo la utalaamu wako na kuwa na orodha kubwa ya baruapepe za watu wanaokufatilia. Hii ni mifano tofauti tofauti ya jukwaa la mwandishi ambao unaweza kuchagua na kuwekeza nguvu hapo na ukauza kitabu chako.
Itaendelea...