- Buy books
- Swahili books
Nitaiambia nini familia yangu
NITAIAMBIA NINI FAMILIA YANGU ni kitabu chenye simulizi inayogusa maisha ya watu wengi kulingana na changamoto za kila siku katika maisha. Niliamua kuandika kitabu hiki baada ya kuona watu wengi wanasahau magumu waliyoyapitia pale mfumo wa maisha yao unapobadilika kulingana na makundi ya watu wanao kutana nao katika maisha. Baada ya mtu kukumbana na changamoto hasi zinazoathiri maisha yake ndipo hugundua kuwa amekosea, hii hupelekea mtu huyo kujiuliza maswali mengi kwamba ataiambia nini familia yake. Hii ni kwasababu, watu wengi huaminiwa na familia zao na kupewa kipaumbele katika maisha, na mara nyingi familia hujitoa kwa hali na mali na kupoteza pesa ili kuhakikisha mtoto anafanikiwa katika maisha yake.
Hivyo basi, kitabu hiki kinatoa angalizo kwa vijana wawe makini katika kuanzisha mahusiano yasiyo rasmi ili wasipoteze mwelekeo wa maisha yao. Kitabu hiki kinajaribu kuonesha mfano wa kijana aliye aminiwa na familia yake na jamii kwa ujumla na aliye tokea familia duni na baadaye akajisahau na kuanza kwenda tofauti na makubaliano kati yake na familia yake. Baada ya kijana huyo kupata matatizo anajuta na kuwaza ataiambia nini familia yake iliyomwamini na kujitoa kwa ajili yake ili aweze kufanikiwa na kuikomboa familia yake.
Pia unaweza kujiuliza kwanini kitabu kimeitwa nitaiambia nini familia yangu? Jina hili la kitabu linasadifu ukweli kwamba familia zetu tunazitia simanzi pindi tunapopata matatizo. Kitabu hiki kinaubunifu wa hali ya juu utakao mfanya msomaji aweze kuburudika, kusikitika, kuumia, kupatwa na huruma na kikubwa zaidi atajifunza mengi yatakayomsaidia katika maisha.
Pia lengo kuu la kuandika kitabu hiki nikuwawezesha vijana kufikia ndoto zao walizojiwekea katika maisha. Kwani kitabu hiki kinamtahadharisha msomaji awe makini na changamoto za mahusiano ili aweze kufikia malengo yake. Pia kitabu hiki kinawasaidia wazazi kujua changamoto wanazokabiliana nazo watoto wao, hivyo wazazi wanaweza kutumia kitabu hiki kama sehemu ya kujua nini chakuwaeleza watoto wao kuhakikisha wanafikia ndoto zao. Kwani wakati mwingine inakuwa vigumu wazazi kupata ujasiri wa kuwaeleza kinagaubaga watoto wao namna ya kuishi katika ujana, kitabu hiki kinaweza kutumika kama shule ya kuwaelekeza watoto na vijana namna bora ya kuishi katika jamii zetu.
Pia kitabu hiki kinaeleza maisha ya wanafunzi wanapoanza masomo yao hadi wakati wa kumaliza masomo yao. Kitabu kimeeleza changamoto anazoweza kukutana nazo mwanafunzi katika ngazi yoyote ya elimu, lakini pia kitabu hiki kimejikita katika maisha ya wanafunzi wa vyuoni ambao hujiona wapo huru pale wanapokuwa vyuoni kitendo ambacho hupelekea kusahau maadili yao na kupoteza mwelekeo sahihi wa maisha yao.
Katika maisha yangu nimekuwa nikifanya utafiti juu ya maisha ya watu pale wanapokuwa mbali na familia zao ndipo nikagundua kuwa watu wengi hubadili mfumo wa maisha yao pale wanapobadili mazingira ya kuishi hasa wanapokuwa mbali na familia zao. Husahau kabisa shida walizopitia na kuanza kuishi kinyume na maadili waliyolelewa au kuelekezwa na familia zao. Hii nidhahiri kuwa watu wengi huficha makucha ya uovu kulingana na taswira ya jamii na familia zao zinavyowachukulia. Baada ya mtu kupata matatizo ndipo huanza kujuta kwa kujiona ni mwenye tuhuma kuikosea maadili familia yake.
Hivyo basi, niliamua kuchukua hatua ya kuandika kitabu hiki baada ya kuona vijana wengi wakikumbana na changamoto za mahusiano katika maisha yao, hivyo nikaamua kuweka bayana namna wanavyoweza kuathiri ndoto zao pia nikajaribu kueleza namna bora yakuweza kutatua matatizo hayo hatimaye familia zijivunie kwa kutoa malezi bora. Kwani ifahamike kuwa maumivu yanayoikumba familia yako unapoharibikiwa ni zaidi ya maumivu unayoyapata wewe mwenyewe. Hivyo familia ikikuamini na kukupa kipaumbele yakupasa kulipa fadhila ya kutoiumiza wala kuifedhehesha kwa kutenda mema yanayo stahiki katika jamii.