Ushauri: Mwandishi wa vitabu fanyia kazi mambo haya 4 ufanikiwe zaidi.
Kwenye tasnia ya uandishi wa vitabu hakuna msahafu mmoja wa kuufuata ili ufanikiwe kwenye uandishi. Kila siku kuna njia mpya na mambo mapya ya kufanya ili uandishi wako uwe na mafanikio. Mara nyingi mafanikio kwenye uandishi wa vitabu ni kuona matunda ya kazi yako na kuyafaidi.
Ni kweli, yapo mambo yasiyobadilika ili mwandishi awe na
mafanikio, hayo ni mambo ya msingi kwenye uandishi wa vitabu. Tumekukusanyia
mambo 4 ya kuongezea kwenye hayo unayojua tayari, huu ni kama ushauri wetu
kwako uweze kufanikiwa zaidi. Mambo hayo ni haya,
1. Andika kitabu kisichochosha. Kama ukiwauliza wasomaji wa vitabu ni jambo gani huwafanya baadhi ya vitabu wakianza kuvisoma hawavimalizi watakwambia kitabu ambacho hakiwapi hamasa na kinachochosha. Kama mwandishi wa vitabu, ushauri wetu ni kuwa, kila unapoandika kitabu kipya, basi hakikisha kitabu chako kuanzia kurasa ya kwanza mpaka ya mwisho kinampa ladha tamu msomaji kiasi kwamba atakiweka chini akiwa amemaliza kusoma. Hapa ndiyo kuna siri ya kutofautisha kitabu kinachouza na kile kisichouza. Fanyia kazi jambo hili na utaona mafanikio.
2. Kuwa mkweli unapozungumzia kitabu chako. Usiwe mmoja ya waandishi ambao anakipamba kitabu chake mno halafu msomaji akinunua anakuta hamna kitu, ni maneno matupu tu ya mwandishi. Kitabu chako kiwe na jalada (kava) bora ambalo litasadifu yaliyomo pia. Usitie chumvi mno huku unajua kitabu chako ni boko boko tu. Ukifanya hivyo, utaathiri mauzo ya kitabu chako kinachofuata, wasomaji watajua ni zile porojo zako kumbe sasa umetoa kitabu kizuri mno. Jambo la muhimu kuwa mkweli na ikiwezekana weka bei ya chini kama unajua kitabu si bora sana. Ukifanyia kazi hili lazima utafanikiwa.
3. Zungumza na wasomaji wako. Kuna waandishi ambao wasomaji wake wakitaka kusema naye jambo hawana namna ya kumfikia. Kama ni kwenye mitandao hajibu meseji za iniboksi, hajibu barua pepe na n.k. Siri ni hii, ukitaka kufanikiwa, chukua ushauri huu, zungumza na wasomaji wako, jichanganye kwenye mitandao hasa Facebook na utaona namna wasomaji wako wanakuwa karibu na wewe zaidi.
4. Pata maoni ya wasomaji na yafanyie kazi. Mara nyingi wasomaji hutoa maoni kwa mwandishi wanapomaliza kusoma vitabu vyao. Sasa ukipata yale maoni yafanyie kazi na wape mrejesho wasomaji wako. Ukifanyia kazi hili, mafanikio yanakuja tu yenyewe.
Umefurahia kusoma chapisho hili? Kuna jambo umejifunza? Tafadhali tuandikie maoni yako kwenye kisehemu cha maoni kinachofuata hapa chini na usisahau ku share na waandishi wengine unaowajua.