Jinsi ya kujenga jukwaa lako kama mwandishi - 2
Kati ya mambo mengi yanayowatatiza waandishi wengi wa vitabu ni kujua maana ya jukwaa la mwandishi ni nini? na jinsi ya kulijenga jukwaa lako kama mwandishi ili kuuza vitabu vyako. Kwa sababu hili ni jambo muhimu kujua, chapisho la leo litajikita kueleza hili kwa kina;
Unajengaje jukwaa lako kama mwandishi?
Katika mifano ya hapo juu, nimegusa mambo matatu, mashabiki wengi ulionao katika mtandao wa kijamii, kujulikana zaidi katika eneo la utalaamu wako na kuwa na orodha kubwa ya baruapepe za watu wanaokufatilia. Hii ni mifano tofauti tofauti ya jukwaa la mwandishi ambao unaweza kuchagua na kuwekeza nguvu hapo na ukauza kitabu chako.
Ikiwa unataka Kujenga jukwaa lako kama mwandishi ili uuzie kitabu chako ukianza na hatua sifuri, fanya mambo haya yafuatayo;
1. Itambue thamani yako. Kitu cha kwanza, itambue thamani yako wewe kama mwandishi. Jiulize upo vizuri kwenye nini? Kitu gani cha pekee kabisa wasomaji watafaidi kutoka kwako?. Kujua thamani yako ni kujua ni kitu gani wewe kama mwandishi unaweka mezani kwa ajili ya msomaji kusoma na hii itaanza kukusaidia wewe kujitofautisha na wengine na kukupa faida ya wasomaji kukujua wewe kama wewe. Mfano, kama wewe ni mwandishi wa riwaya, ubora wako na ladha yako ya pekee inayokutofautisha na waandishi wengine wa riwaya utakupa watu watakaokupenda na kukufatilia, na huo ndiyo mwanzo wa wewe kuanza kujenga jukwaa lako. Thamani yako itakuweka mbele ya wasomaji watakaokuwa mashabiki wako
2. Anza kuchunguza mawasiliano yako. Angalia katika orodha ya nambari za mawasiliano uliyonayo na uone nani unamjua ambaye tayari amepiga hatua kuliko wewe? Nani unamjua anayemjua mtu anayeweza kukusaidia wewe kupiga hatua ya kuuza zaidi kitabu chako?. Mfano ukawa na mawasiliano ya mhariri wa gazeti fulani, mtangazaji wa kituo fulani cha TV au redio?, blogger fulani maarufu?. Kama umekosa huku kote, jiulize tena, ni mwandishi gani mkubwa ambaye ukiunganishwa naye ataweza kukusaidia? Kama kote umekosa kabisa, jambo la mwisho unaweza kufanya ni, andika katika ukurasa wako wa mtandao wa kijamii mfano Facebook, “Nani anaweza kukusaidia kupata mawasiliano ya mtangazaji wa kipindi fulani katika kituo fulani cha TV au redio?”. Ukiwa na mtu mwingine wa kukushika mkono na kukusaidia, basi safari yako ya kutengeneza jukwaa lako inakuwa rahisi zaidi na yenye nafasi ya kupata mafanikio zaidi
3. Jenga mtandao. Unataka mtandao wako wa watu wa aina gani? Mtandao huu wa watu ndiyo watu wanaokuwa katika jukwaa lako, na ndiyo watu watanunua kitabu chako kwa sababu wanakujua, wanakufatilia na kukupenda. Sasa unapojenga mtandao huu, hakikisha unakuwa na watu ambao watakuwa na wewe hata unapoendelea kutoa kutoa vitabu vingine hapo baadaye. Mtandao bora zaidi ni kuwa na orodha ya baruapepe za watu wako kwa sababu unakuwa na umiliki wa asimilia mia moja tofauti na kuwa na mashabiki wa mtandaoni. Sasa utapataje hizo baruapepe zao, hii ni topiki nyingine kabisa, lakini kwa kuanza, unaweza soma kozi ya Jinsi Kuandika na Kutoa eBook kutoka DaudiPages.
4. Jukwaa lako unataka liweje?. Hili ni jambo la mwisho muhimu sana. Namna vile jukwaa lako litakuwa ni vile wewe utakavyokuwa karibu na watu wako na kuhusiana nao. Vitu gani wanataka kwako? Vitu gani unawapatia? Unawapatiaje hivyo vitu? Haya ni maswali muhimu ambayo lazim uwe na majibu yake.
Jukwaa mbili huwa hazifanani
Nataka ukumbuke jambo hili kuwa, jukwaa la mwandishi huyu na yule hayatafanana kabisa. Ndiyo maana ni muhimu kujua wewe kama mwandishi unataka kujenga jukwaa la namna gani?