HATUA TANO ZA KUWATAMBUA WASOMAJI WAKO WALENGWA.
Mafanikio ya kutangaza kitabu chako yamejificha kwenye kumjua msomaji wako mlengwa na kumpatia anachotaka.
Unaposhindwa kumjua msomaji wako mlengwa unaangukia kwenye mtego wa kumwambia kila mtu kuhusu kitabu chako na utajaribu kuwepo kila mahali unapoona unaweza kupata watu. Kwa bahati mbaya utapata matokeo kidogo na yamkini ukakata tamaa kwamba kitabu chako hakiuzi.
Unapomjua msomaji wako mlengwa inapata matokeo unayotaka na unaachana na mambo ya kubahatisha bahatisha.
Swali la msingi linabaki, unaweza kumtambua msomaji wako mlengwa? Zipo hatua tano zifuatazo ambazo unapaswa kuzifanyia kazi;
1. Anza na kitabu chako. Umeandika kitabu cha aina gani? Ni riwaya ama kitabu cha kiroho au pengine ni kitabu cha biashara? Hapa ndipo pa kuanzia ili ujue sasa kitabu chako kina vitu gani ambavyo ni kama sumaku ya kuwavuta watu wanaopenda aina ya kitabu ulichoandika.
2. Kitu gani cha pekee wewe unacho. Waandishi waloandika riwaya ni wengi, Je! Wewe utofauti wako ni upi? Ni kipi wewe umeweka mezani ambacho msomaji akiona atavutika na uandishi wako?. Ni muhimu sana wewe kama mwandishi ujijue, ujue mtindo wako wa uandishi [Soma kozi ya bure ya kufahamu mitindo ya uandishi hapa] na n.k.
3. Nani atasoma kitabu chako?. Wasomaji wako wengi lakini ni nani ambaye atasoma cha kwako?. Unaweza kuangalia waandishi wengine wanaoandika kitabu kama cha aina yako ili ikusaidie kujua aina ya msomaji ambaye kwako atanunua.
4. Tengeneza picha ya msomaji wako vile atakuwa. Pengine hii ndiyo hatua ngumu zaidi. Hapa unatakiwa mchore chini yule msomaji unafikiri atakuwa ndiyo mlengwa kusoma kitabu chako. Baadhi ya maswali ya kujiuliza unapomchora msomaji wako
a. Ana umri wa miaka mingapi?
b. Ni mwanamke ama mwanaume?
c. Anafanya kazi gani?
d. Umeoa/kuolewa ama yupo bachela?
e. Ana kipato gani?
5. Fanya majaribio. Baada ya kumtengeneza msomaji wako mlengwa katika hatua ya 4, sasa anza kumjaribu kama atakuwa hivyo au la!. Baadhi ya njia za kufanya majaribio ni hizi;
a. Tumia sumaku ya kumnasa msomaji kama vile kutoa kitabu bure, kuweka punguzo na n.k. Msomaji mlengwa atamahasika kuchukua kitabu.
b. Jiunge na makundi ya wasomaji ya Facebook au WhatsApp. Weka vitu vyako huko na msomaji mlengwa atahamasika kujua zaidi.
c. Andika chapisho na weka kwa blogi yako ama blogi ya muandishi mwingine na angalia wasomaji wanaofurahia kusoma n ahata kukupa mrejesho
d. Rekodi podikasti na alika wasikilize. Msomaji mlengwa atahamasika tu.
Unapofanya haya majaribio, hakikisha unaweka rekodi, njia inayofanya kazi endelea kuitumia na iboreshe zaidi, ile inayofeli achana nayo.