Utambulisho katika Kristo
Kila jambo ambalo mtu analifanya analifanya kutokana na jinsi yeye mwenyewe anavyojitambua. Mfano binafsi, ni kwamba nimefanya mambo mengi sana katika maisha yangu, mazuri na mabaya na mambo hayo yote niliyoyafanya niliyafanya kutokana na vile nilivyojiona niko.
Wakati mwingine nilijiona kama mtu wa kawaida, kama mnyama, yaani, kama kuku, au ng’ombe, au mbuzi, au pundamilia, au mbwa. Nataka kukwambia kwamba, sikujiona katika hali hizo makusudi, lakini ndani yangu nilifanya tu mambo yale ambayo wanyama hao wanayafanya, nikayazoea na hatimaye yakawa ndiyo mimi. Hali hii iliniingia kwa unyemelevu kiasi kwamba sikuwa najitambua kwa makusudi na nilipoteza kabisa udhibiti wa nafsi yangu.
Si vigumu kufanya mambo wanayofanya wanyama endapo na wewe mwenyewe haujioni kama u-tofauti nao.
Nilipokuwa shule ya sekondari nilijiona kama mmoja wa wanamziki wa miziki ya hiphop wa kule Marekani. Tabia za hawa wanamziki kwa ujumla ni hasira, kisasi, dharau, mashindano na kiburi. Hivyo, na mimi nikawa na tabia hizo hizo, nikafanya kwa jinsi nilivyoweza kufanya kama vile wao walivyofanya; kudharau watu, kukasirikia wengine bila kujali umri au jinsia, kushindanashindana tu, alimradi na mimi nionekane nipo.
Hayo yote niliyafanya ili nitambuliwe. Yumkini, sikuwa na utambulisho wangu thabiti, hivyo, utambulisho wowote ule uliokuja mbele yangu ulinifaa. Na sikuwa na mwongozo uliokuwa na nguvu kuniwezesha kuwa na msimamo wangu mwenyewe. Hivyo niliishia kufanya mambo mengi ambayo yaliiharibu sana nafsi yangu.
Yapo pia mambo mazuri niliyojitambulisha nayo; nilipomaliza masomo nilipata nafasi ya kusoma kitabu kimoja kilichonisaidia sana. Mwandishi wa kitabu hicho alielezea mambo kadhaa ambayo aliyaweka kama msingi wa mtu kufanikiwa katika maisha yake bila kujali maisha yake ya siku za nyuma.
Mwandishi alisistiza kwamba kila kitu ambacho mtu anakitaka anaweza kukipata alimradi amekifikiria tu; yaani ukifikiria na kujega taswira ya kitu unachokitaka, ukaamini kwa mkazo wote, utakipata.
Nilikisoma kitabu hicho karibu kila siku mwanzo mwisho. Kilinisaidia sana kubadilisha mtazamo wangu.
Hivyo ni wazi kwamba, jinsi mtu anavyojiona, anavyojidhania; yeye mwenyewe binafsi kwanza, ni muhimu sana katika maisha yake yote.
Sasa, jinsi hii ya kujiona au kujidhania ndiyo utambulisho wa mtu. Hakuna mtu mwingine yeyote anayeweza kumbadilishia mtu utambulisho wake isipokuwa mtu huyo amekubali na amekusudia kabisa kuubadilisha utambulisho
Recommended for you

