Hamasika Kila Siku
Kufanya kitu kimoja kwa kukirudia, ndio kitu kigumu ambacho kina changamoto kubwa katika kuleta mabadiliko ya watu wakati wa kuchukua hatua kwenye maisha ya kila siku. Kwani tafiti zinasema, watu wengi wanaweka malengo mwanzo wa mwaka, kufikia tarehe 19 ya mwezi wa kwanza, nusu ya watu wanakuwa tayari wamesahau na kuachana na malengo ambayo walikuwa wameyaweka mwanzo wa mwaka.
Ukifuatilia kwa kiasi kikubwa, kitu kinachosababisha mwendelezo huo kukwama ni hamasa inayokosekana katika kufanya kitu cha mwendelezo wa kila siku hata kwa hatua kidogo. Msingi wa kitabu hiki cha Hamasika kila siku ni kukuchambulia kila eneo la maisha ambalo linatuzunguka na kukutengea tafakari 366; ambazo ni moja kwa siku; namba za mwaka mrefu ambao unatoa kwenye mzunguko wa mwaka. Ukiweza kuandika kila siku hata tafakari moja na kuisoma mfululizo, kitu hicho kimoja tu kinakwenda kuleta mabadiliko kwenye maisha yako. Kwani tabia moja ndogo inaleta athari kwenye vitu vingine unavyovifanya kwenye maisha yako. Ukiweza kusoma Tafakari hizi za Hamasa kila siku, kwa siku ishirini na moja mfululizo utaweza kutengeneza tabia nyingine; ambayo utaweza kuichagua ili kufanya makubwa hata kwa hatua ndogo ndogo kwenye maisha yako.
Chukua muda kujisomea kitabu hiki angalau tafsiri moja tu kila siku katika mwaka na kuitafakari na unaweza kurudia kila mwaka. Hapo utapata nguvu ya kuweza kufikia mafanikio makubwa kwa hatua ndogondogo unazozifanya kila siku. Katika maisha, kuchukua hatua ni jambo linalopaswa kufanyiwa kazi mara zote ili kuweza kutimiza malengo na ndoto kubwa tulizojiwekea. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuliona kusudi na maana ya maisha yetu hapa duniani.
Licha ya kila mtu kutamani mafanikio kwenye maisha, lakini ni wachache sana walioshinda katika hili. Sababu kubwa inayotofautisha makundi haya mawili, si nyingine bali ni uthubutu wa kuchukua hatua na mwendelezo. Kitabu hiki sasa kinaenda kuwa mwarobaini, kwa kukupa tafakuri ambazo unaweza kuzisoma kila siku unapoamka. Unasoma ili uendelee kuwa na motisha na hatimaye kutimiza malengo yako kwa wakati mwafaka uliojiwekea.
Kwa namna nilivyoandaa tafakuri hizi, ninashauri kila siku ukiamka asubuhi usome angalau moja. Hii itakusaidia kuianza siku yako kwa hamasa na kuiendeleza kwa ushindi. Kifanye kitabu hiki kiwe rafiki kwako na kisome kila siku bila kuacha kwa mwaka mzima. Ninakuhakikishia kitu kimoja, kama utafanyia kazi utakayokuwa unajifunza humu, hutapoteza hamasa yako wala kushindwa kufanikisha malengo yako. Kama vile ilivyo nguvu ya tabia, kitu kimoja ukikirudia kukifanya mara nyingi kinaambukiza tabia nyingine kwenye ufanyaji wa hicho kitu. Hapo utaweza kupiga hatua kwenye zile tabia ambazo zinahitaji hali ya kurudiarudia kama vile uwekaji wa akiba, ufanyaji mazoezi, uandishi wa vitabu na vitu vinginevyo vinavyotaka kurudiwarudiwa. Ninakutakia usomaji mwema. Ninaamini upo tayari kubadilika na maisha yako hayatakuwa vile ulivyo sasa baada ya kusoma kitabu hiki. Nikupongeze kwa hatua kubwa na muhimu uliyoichukua ya kukipata kitabu hiki endelea kukisoma ili kujipatia mahitaji Hamasa muhimu ya kila siku kukuwezesha kupata mafanikio makubwa.
Naamini hutajutia maamuzi yako ya kukipata kitabu hiki, nakutakia kila la kheri katika usomaji na uchukuaji hatua.
Recommended for you

