Safari ya Kumjua Mola Wangu
Katika historia ya mwanadamu, hakuna jambo lililo hatari zaidi kwa nafsi yake kuliko kumsahau Muumba wake. Ni kusahau ambako hakutokani na ukosefu wa ushahidi, bali ni kupotea kwa dira ya kiroho. Watu wengi wamezama katika bahari ya maarifa ya kimaada, wakipima nyota kwa darubini na kuchunguza chembe ndogo kwa hadubini, lakini wakashindwa kuona alama kuu iliyo wazi zaidi: kwamba kila kitu kilichopo ni ushahidi wa uwepo na utukufu wa Muumba.
Mwenyezi Mungu, kwa hekima Yake, hakuwapa wanadamu akili kwa ajili ya biashara ya dunia pekee, bali kama chombo cha kutambua ukweli wa juu zaidi. Ndiyo maana katika Qur’an Tukufu, amewaamrisha mara nyingi watumie akili zao kuchunguza uumbaji:
“Hakika katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya usiku na mchana, zipo ishara kwa wenye akili.” (Aal Imran, 3:190)
Aya hii si mwaliko wa kimaandishi tu, bali ni amri ya kiroho na kielimu: kwamba uchunguzi wa kisayansi, unapofanywa kwa unyenyekevu na kwa nia safi, ni ibada. Sayansi, kwa mtazamo wa kiwahyi, ni njia ya kumtambua Muumba, si kisingizio cha kumkana. Lakini katika zama hizi, wengi wameigeuza kuwa kivuli cha kujitukuza, wakidhani kuwa kugundua kanuni za maumbile ni sawa na kumiliki mamlaka juu yake wakisahau kwamba kanuni hizo ni sehemu ya mpangilio wa Yule Aliye zipanga.
Kitabu hiki kimekusudiwa kuwa daraja kati ya maarifa na ibada; kati ya uchunguzi wa kisayansi na kiroho.
Msomaji mpendwa, karibu katika safari ya tafakuri na utafiti; safari ya kuondoa vumbi la kutokujua, na kuingia katika mwangaza wa maarifa yanayo mrejesha mwanadamu kwa Muumba wa ulimwengu wote.
Others Also Bought